Search This Blog

Thursday, September 26, 2013

SERIKALI YAOMBA MSAANDA KUENDELEZA MICHEZO KWA VIJANA HASA WANAFUNZI

 Waziri wa habari  vijana na Utamaduni na Michezo Dk Fenella Mukangaraakipokea kombe ikiwa ni sehemu vifaa vya michezo kutoka kwa mkuu wa masoko wa  Vodacom Kelvin Twissa Dar es salaam jana vitakavyotumika katika mashindano yatakayoshirikisha timu 12 za sekondari kutoka manispaa za jijin humo.


SERIKALI imekabidhiwa vifaa vya michezo vyenye thamani ya Sh milioni 11 na Kampuni ya Vodacom Tanzania kwa ajili ya kuendeleza michezo shuleni. Vifaa alivyokabidhiwa ni pamoja na jezi seti 12, mipira 40 na kombe moja kubwa kwa ajili ya zawadi.

Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa vifaa hivyo, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk Fenella Mukangara alisema vifaa hivyo watavitumia katika mashindano ya mpira wa miguu yatakayoshirikisha timu 12 kutoka shule za Sekondari Ilala, Temeke na Kinondoni, yatakayotangazwa Oktoba mwaka huu.

Alisema wamechagua shule chache za Dar es Salaam kama sehemu ya kuanzia, ila wanajipanga na kuhimiza wadau wengine wajiunge kwa kadri ya uwezo, ili vijana walioko hadi vijijini waweze kushiriki kikamilifu.

“Naomba nitoe wito kwa kampuni mbalimbali kusaidiana na serikali katika kuhakikisha tunawafanya vijana na hasa wanafunzi kuwa tegemeo la Taifa kwa sasa na baadaye katika maendeleo ya sekta zote kupitia michezo,” alisema.

Dk Mukangara alisema msingi wa michezo mahali popote pale duniani ni vijana wadogo kushiriki katika shughuli za michezo tangu hatua za awali kabisa za makuzi na elimu, hivyo maendeleo ya soka yatatokana na uwekezaji wa makusudi wa kukuza soka na michezo mbalimbali shuleni.
 
Alisema serikali ingependa kuona vijana, watoto wote na wakubwa wanacheza katika kujenga miili, lakini ni muhimu kufanya maamuzi ya makusudi ya kuwekeza kwanza katika michezo.

Hili ni kutokana na ukweli kuwa kuendesha shughuli za michezo ni ghali na hivyo si suala la serikali peke yake, bali wadau wote, makampuni, mashirika ya umma na binafsi kuwekeza huko ili kupata timu bora zaidi katika ngazi ya Taifa kwa michezo mbalimbali,”alisema.

No comments:

Post a Comment