Search This Blog

Friday, September 27, 2013

JAMII YAHIMIZWA KUWASAIDIA WATOTO ILI WAWEZE KUPATA ELIMU
















Na Anna Nkinda – Maelezo, New York

26/9/2013 Ilielezwa kwamba ikiwa kila mtu atatimiza wajibu wake katika jamii hakutakuwa na mtoto atakayekosa elimu kwa ajili ya kutokuwa na ada, vitabu na nguo za shule pia hakutakuwa na watu watakaokufa kwa kukosa  chakula na malazi.

Ili kuhakikisha hayo yote yanafanikiwa jitihada za pamoja zinahitajika kwa wadau wote wa maendeleo  kufanya kazi kwa pamoja na kushirikiana ili waweze kutimiza malengo na mipango waliyojiwekea.

Hayo yasemwa jana na mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akiwasilisha mada kuhusu uvumilivu na uongozi wa wanawake wa Afrika katika kukabiliana na changamoto za kibinadamu kwenye mkutano maalum wa kujadili utekelezaji wa huduma za kibinadamu barani Afrika uliofanyika mjini New York nchini Marekani.

Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema kupatikana kwa elimu bora kwa mtoto kutamwezesha  kupata fursa mbalimbali ikiwa ni pamoja na afya bora, kuongezeka kwa kipato cha familia na hivyo kujikwamua na  hali ya umaskini.

“Kitaaluma mimi ni mwalimu nafahamu changamoto zinazowakabili watoto na familia zao wakati wanajitahidi kupambana na ujinga, magonjwa na maisha ya umaskini  kutokana na hali hii, mimi naona kuwapatia elimu ni njia moja wapo itakayowafanya waweze kuepukana na umaskini kwani mara wamalizapo masomo yao wataweza kupata ajira na hivyo kujitegeme”, alisema Mama Kikwete.

Mwenyekiti huyo wa WAMA aliwaambia wajumbe waliohudhuria mkutano huo kuwa aliamua kuanzisha taasisi hiyo ambayo kupitia kwake ameweza kuhakikisha watoto wa kike wanakwenda shule kwa kuwajengea mazingira mazuri ya kusoma kwani mtoto wa kike akikaa shule muda mrefu ndivyo anavyoweza kuepukana na mimba za utotoni, vifo wakati wa kujifungua na hali ya umaskini.

Mama Kikwete alisema, “kutokana na hali hii tumejenga shule ya sekondari ya mfano ya WAMA-Nakayama iliyopo wilaya ya Rufiji mkoani Pwani ambayo inatoa elimu bure kwa watoto wa kike ambao ni yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi nia ya kuanzisha shule hii yenye wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha nne  325 ni kuwapatia watoto hawa elimu sawa na wenzao ambao wanawazazi.

Kazi nyingine zinazofanywa na Taasisi hiyo ni kuwawezesha wanawake kiuchumi kwa kuwapatia elimu ya ujasiriamali na kuwaongezea mitaji ya biashara  na kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo wanatarajia kuwafikia wanawake 60000.

Pia wanahakikisha vifo vya kina mama wajawazito na watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano vinapungua kwa kutoa elimu kwa jamii jinsi gani inaweza kuepukana na maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto na kutoa elimu ya jinsia na uzazi kwa vijana ili waweze kuepukana na mimba za utotoni na ugonjwa wa Ukimwi.

Akifungua mkutano huo Mjumbe maalum wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia unyanyasaji wa kijinsia na utatuzi wa migogoro Zainabu Bangura alieleza kwamba katika bara la Afrika wanawake wanazalisha mali kwa asilimia 70 ya uchumi usio rasmi na asilimia 20 kwa  uchumi rasmi hivyo basi kuwanyanyasa, kuwabagua, kuwakandamiza na kuwadidimiza wanawake ni sawa na kudidimiza taifa zima.

Msemaji Mkuu katika mkutano huo kutoka Umoja wa Afrika (AU) Aisha Abdullahi ambaye ni Kamishina anayeshughulikia masuala ya siasa   alisema kuwa pamoja na ukweli kwamba ndani ya Bara la Afrika  kuna utashi mkubwa wa kisiasa na nia ya kushughulikia changamaoto za masuala ya kibinadamu, bado bara hilo linakabiliwa na idadi kubwa ya wakimbizi wa ndani na nje zaidi ya million 15.

Abdhullahi alisema, “Wakimbizi hawa wanahangaika kutafuta  mavazi, chakula na makazi maeneo mbalimbali ya Bara la Afrika. Pamoja na changamoto nyingine za umaskini, uchumi duni na matatizo ya kisiasa katika baadhi ya nchi  Umoja wa Afrika umeliweka suala la wakimbizi kuwa ni moja ya  agenda zake muhimu”.

Mkutano huo ulioandaliwa na ofisi za umoja wa Mataifa inayoratibu masuala ya kibinadamu (OCHA) na kuhudhuriwa na wajumbe mbalimbali kutoka ofisi za taasisi za kimataifa na kikanda.

Thursday, September 26, 2013

SERIKALI YAOMBA MSAANDA KUENDELEZA MICHEZO KWA VIJANA HASA WANAFUNZI

 Waziri wa habari  vijana na Utamaduni na Michezo Dk Fenella Mukangaraakipokea kombe ikiwa ni sehemu vifaa vya michezo kutoka kwa mkuu wa masoko wa  Vodacom Kelvin Twissa Dar es salaam jana vitakavyotumika katika mashindano yatakayoshirikisha timu 12 za sekondari kutoka manispaa za jijin humo.


SERIKALI imekabidhiwa vifaa vya michezo vyenye thamani ya Sh milioni 11 na Kampuni ya Vodacom Tanzania kwa ajili ya kuendeleza michezo shuleni. Vifaa alivyokabidhiwa ni pamoja na jezi seti 12, mipira 40 na kombe moja kubwa kwa ajili ya zawadi.

Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa vifaa hivyo, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk Fenella Mukangara alisema vifaa hivyo watavitumia katika mashindano ya mpira wa miguu yatakayoshirikisha timu 12 kutoka shule za Sekondari Ilala, Temeke na Kinondoni, yatakayotangazwa Oktoba mwaka huu.

Alisema wamechagua shule chache za Dar es Salaam kama sehemu ya kuanzia, ila wanajipanga na kuhimiza wadau wengine wajiunge kwa kadri ya uwezo, ili vijana walioko hadi vijijini waweze kushiriki kikamilifu.

“Naomba nitoe wito kwa kampuni mbalimbali kusaidiana na serikali katika kuhakikisha tunawafanya vijana na hasa wanafunzi kuwa tegemeo la Taifa kwa sasa na baadaye katika maendeleo ya sekta zote kupitia michezo,” alisema.

Dk Mukangara alisema msingi wa michezo mahali popote pale duniani ni vijana wadogo kushiriki katika shughuli za michezo tangu hatua za awali kabisa za makuzi na elimu, hivyo maendeleo ya soka yatatokana na uwekezaji wa makusudi wa kukuza soka na michezo mbalimbali shuleni.
 
Alisema serikali ingependa kuona vijana, watoto wote na wakubwa wanacheza katika kujenga miili, lakini ni muhimu kufanya maamuzi ya makusudi ya kuwekeza kwanza katika michezo.

Hili ni kutokana na ukweli kuwa kuendesha shughuli za michezo ni ghali na hivyo si suala la serikali peke yake, bali wadau wote, makampuni, mashirika ya umma na binafsi kuwekeza huko ili kupata timu bora zaidi katika ngazi ya Taifa kwa michezo mbalimbali,”alisema.

SIKU YA UNYWAJI MAZIWA MASHULENI























Baadhi ya wanafunzi wa shule mbalimbali za msingi mkoani Iringa wakiwa kwenye maandamano kuadhimisha Siku ya Maziwa Shuleni ambapo kitaifa imefanyika mkoani Tanga.

Friday, September 20, 2013

OPERESHENI KIBUNGA SASA YAHAMIA WIZARA YA ELIMU



















Pichani Katibu mkuu wachama cha Mapinduzi(ccm)Abdulrahman Kinana 


Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa na Naibu wake, Philipo Mulugo wametakiwa kushughulikia  madeni ya walimu haraka iwezekanavyo ama endapo  watashindwa kutatua madai ya walimu basi safari yao  haitakuwa ndefu kwenye sekta hiyo .

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana hapo juzi akiwa Bariadi na jana katika eneo la Lamadi wilayani Busega, Kinana alisema umefika wakati kama waliopewa jukumu la kushughulikia matatizo ya walimu wameshindwa kutimiza majukumu yao wakaachia ngazi ili wengine washike nafasi hizo.

Hali hiyo inatokana na kukithiri kwa madai ya watumishi wa sekta ya elimu ambapo Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana amekerwa na tabia ya walimu kutolipwa fedha zao na kusababisha kuendelea kudai madeni kila kukicha.

Amesema Rais Jakaya Kikwete alitoa agizo la madeni ya walimu kumalizwa na endapo hakuna fedha mwalimu asihamishwe huku akilalamika kuwa kama wasimamizi wa sekta hiyo wameshindwa kusimamia majukumu yao waachie ngazi. 

Katibu huyo alionesha kutofurahishwa na namna madeni ya walimu yanavyoongezeka bila kutafutiwa ufumbuzi na kuitaka wizara hiyo kutafuta ufumbuzi wake na iwapo watashindwa kumaliza madai ya walimu ndani ya miezi sita ataitisha kikao cha wabunge wa CCM kushinikiza wasimamizi wa wizara wajiuzulu.

“Tunataka ndani ya miezi sita madeni ya walimu yawe yamepata ufumbuzi, hatuwezi kila siku tunasikiliza walimu wakilalamika halafu waliopewa dhamana wanashindwa kutafuta ufumbuzi wake.

MBARONI KWA TUHUMA ZA KUWALAWITI WANAFUNZI























Jeshi la Polisi mkoani Iringa linamshikiliwa mwalimu wa shule ya Shule ya Sekondari Wanging’ombe, mkoani Iringa , kwa tuhuma za kuwalawiti wanafunzi

Kamanda wa Polisi mkoani Iringa Ramadhan Mungi amesema kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa Septemba 13, mwaka huu, majira ya saa 10 jioni, akiwa kwenye nyumba anakoishi eneo la Don Bosco. 

Hata hivyo, amesema mwalimu huyo pia ni mwanafunzi wa mwaka wa kwanza Chuo Kikuu cha Mkwawa, anatuhumiwa kuwalawiti wanafunzi wanne ambao  alikuwa akiwarubuni kwa fedha kiasi cha sh. 200 ili wasifichue siri ya unyama wake huo.

 Amesema mwanafunzi mmojawapo kati ya waliolawitiwa, ndiye aliyewaongoza polisi hadi nyumbani kwa mshtakiwa na kuwaonesha chumba walichofanyiwa kitendo hicho.

Mungi amesema kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na kwamba jalada lake limetumwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kutoa uamuzi zaidi ikiwamo mtuhumiwa huyo kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili za kuwalawiti wanafunzi.

Kutokana na hali hiyo Wanaharakati wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), na Kituo cha Msaada wa Kisheria kwa Wanawake na watoto Mkoa wa Iringa wamelipongeza Jeshi la Polisi kwa kumkamata mwalimu na mwanafunzi wa Chuo cha Elimu Mkwawa Iringa anayedaiwa kuwalawiti wanafunzi wanne wa shule ya msingi mkoani Iringa.

Naye Mwanasheria wa Kituo cha Msaada wa Kisheria kwa Wanawake na Watoto Mkoa wa Iringa, Jackson Gaso akizungumza na mwandishi wa habari hizi mjini hapa juzi, alisema kuwa hatua zilizochukuliwa na jeshi la polisi mkoa kumsaka na kumkamata mtuhumiwa huyo ni hatua za kupongezwa.

Amesema kuwa iwapo polisi wangenyamaza kimya vitendo vya ukatili na kinyama vitaendelea kushika kasi mkoani Iringa.

“Kwa dhati nampongeza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Ramadhan Mungi na askari wote ambao wameshiriki kumkamata mtuhumiwa huyo.

Ila tunaomba upelelezi ukamilike mapema ili mhusika afikishwe mahakamani ili iwe fundisho kwa wengine,” alisema Gaso.

Jeshi hilo linaendelea kumshikilia mwalimu huyo anayefundisha katika Shule ya Sekondari Wanging’ombe, iliyopo Wilaya ya Wanging’ombe, mkoani Njombe,  Mwasile Cletus (31).  

Mwalimu huyo anadaiwa kuwalawiti wanafunzi wanne wa shule ya msingi mjini Iringa wakiwemo wanafunzi wa darasa la nne ambao majina na shule zao  zimehifadhiwa.












UGANDA WALIMU NAO WAGOMA SHULE ZAFUNGWA


















Mara baada ya sintofahamu kuhusu walimu huko nchini kenya hatimae wingu  la migomo limeendelea kutokea ambapo nchini Uganda shule zimefungwa baada ya walimu kugoma kwa siku nne mfululizo.  

Katibu mkuu wa Chama cha Walimu Uganda alisisitiza kuwa hawataingia madarasani hadi Serikali itakapowaongezea asilimia 20 ya mishahara yao. 

Walimu hao wamelalamikia mishahara midogo, suala ambalo limewafanya zaidi ya wanafunzi milioni 12 kushindwa kuingia madarasani hivyo kushindwa kupata elimu.

 Awali Serikali ya Uganda iliahidi kuongeza mishahara ya walimu kwa awamu tatu yaani asilimia 15 katika mwaka wa fedha uliopita, asilimia 20 mwaka huu na asilimia 15 mwaka ujao.

Hata hivyo ilikiri haina fedha za kulipa nyongeza ya asilimia 20 ya mishahara ya walimu.

Saturday, September 14, 2013

PICHA NA MATUKIO MBALIMBALI YA WANAFUNZI WA SHULE SECONDARY ST.TERESA KUTOKA SAME WAKIWA REDIO MWAMBAO FM

















Huu ni usafiri walioutumia wanafunzi wa St Teresa iliyopo Same kilimanjaro hadi Tanga

















Huu pia usafiri walioutumia wanafunzi wa St Teresa iliyopo Same kilimanjaro hadi Tanga

















wenyewe hao
 

wakiwa kwenye mosheni


Aliyevaa tshit nyeusi ni Mtangazi wa kipindi cha burudani kiitwacho Bongo Babkubwa Make Manyanga akijiandaa andaa kabla ya kuvamiwa na wanafunzi hao

















Wakifurahia mazingira ya studio za Redio Mwambao fm Tanga kalba ya mahojiano maalumu juu ya kipindi cha Mimi na Mwanafunzi

Baadhi ya wanafunzi wa St Teresa kutoka Same wakiwa katika mahojiano maalumu na mtangazaji wa kipindi cha Mimi Na Mwanafunzi Suleiman Kibugo aliyefalia suruali kadet
Haya mazingira mazuri jamani yametufahisha (maneno ya wanafunzi hao)


Friday, September 13, 2013

SERIKASLI YAOMBWA KUBORESHA KAMBI ZA WANAFUNZI














Wanafunzi waliomaliza mitihani yao ya darasa la saba wameiomba serikali kuboresha kambi walizokuwa wamewawekea kufundishwa ziendelezwe hadi shule za sekondari.

Wakizungumza na Mimi na Mwanafunzi  baada ya kumaliza mtihani wa mwisho wanafunzi wa shule ya msingi Chanika wilayani Handeni mkoani Tanga  wameshukuru kambi hizo kwani zimekuwa na faida kwao katika mitihani waliofanya.

Rashidi Rajabu mwanafunzi wa shule ya msingi Chanika amesema kuwa kambini walikuwa wakifanya majaribio mara kwa mara hali iliyowafanya kujiongezea ujasiri wakutoogopa mitihani.

Akiongelea suala hilo Afisa Taaluma Sekondari  wilaya ya Handeni, Basil Mrutu amesema mpango huo  wa kuanzisha kambi hizo kwa sekondari katika robo ya tatu ya mwaka huu wa fedha 2013-2014 kwa sekondari zote za sekondari wilayani humo upon a utaanza.

Mrutu amewaomba wazazi washirikiane na viongozi wa shule katika kutoa chakula cha mchana kwa kuchangia fedha kidogo ili wanafunzi wapate chakula shuleni.

ELIMU YA MSINGI IWE KIDATO CHA NNE
















Waziri wa elimu na mafunzo ya Ufundi Dk Shukuru Kawambwa

Wakati Wanafunzi wa darasa la saba nchini kote jana walimaliza kufanya mtihani wa kuhitimu masomo ya elimu ya msingi.

Tunafarijika kusikia kwamba mtihani huo ulifanyika katika mazingira ya amani na utulivu karibu nchi nzima, jambo ambalo pengine linadhihirisha kwamba Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imejifunza kutokana na makosa yaliyofanyika huko nyuma,  hivyo taratibu inaanza kutupeleka kule tunakotaka kwenda.

Kutokana na ukubwa wa nchi yetu, bado ni mapema mno kusema kwamba mambo yote yalikwenda kama ilivyopangwa, ingawa wahenga walisema siku njema huonekana asubuhi.

Tulizoea kupata habari mbaya za mambo mengi kwenda mrama kila mtihani huo ulipokuwa ukifanyika, ikiwa ni pamoja na wizi wa mitihani, kucheleweshwa kwa vifaa, wasimamizi kutofika vituoni walikopangiwa na kadhalika.

Kwa siku mbili mfululizo, viongozi wa wizara hiyo katika ngazi zote nchini, wakiwamo Waziri, Dk Shukuru Kawambwa na Naibu wake, Philipo Mulugo walikuwa wakizunguka katika shule mbalimbali kuhakikisha mtihani huo ulikuwa ukifanyika katika hali inayokubalika.

Hii ni tofauti na miaka ya nyuma ambapo viongozi wengi walikuwa wakikaa katika ofisi zenye viyoyozi wakisubiri kuletewa taarifa za mwenendo wa mitihani hiyo, pasipo kujua kwamba taarifa nyingi zilikuwa za kubuni na nyingine zilikuwa zimechakachuliwa.

Kinachotakiwa sasa ni Wizara kujielekeza zaidi katika kutatua matatizo yanayokwamisha elimu ya msingi, badala ya kuridhika tu na mipango, matamko na mikakati sio tu isiyoendana na vitendo, bali pia isiyotekelezeka hata kama inafanywa kwa nia njema.

Kwa mfano, Wizara inaonekana kama imepagaa na ‘Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa’ ambao, pamoja na kufanikiwa katika nchi nyingine kama Malaysia, inabidi tafsiri na utekelezaji wake ufanywe kwa kutilia maanani mazingira tuliyomo.

Mpango huo lazima uwe na dira ili uweze kutekelezeka. Kwa mfano, wanafunzi zaidi ya 800,000 waliomaliza jana elimu ya msingi walitayarishwaje ili elimu hiyo iwawezeshe kumudu maisha yao? Je, elimu hiyo inatosha au taifa lijielekeze sasa katika kufanya elimu ya msingi kuwa kidato cha nne?  Mwaka jana wanafunzi asilimia 64 tu waliofanya mtihani huo ndio waliochaguliwa kwenda sekondari, huku asilimia 36 ikiachwa kutokomea mitaani kueneza ujinga na kugawana umaskini.

Bahati mbaya Waziri Kawambwa bado ni mateka wa takwimu zinazompa ndoto za kufaulisha wanafunzi 80 kati ya 100 ifikapo mwaka 2015 katika elimu ya msingi.

 Alikaririwa juzi akisema mwaka huu ufaulu utaongezeka kutoka asilimia 31 hadi asilimia 60 na kwamba ongezeko hilo litakwenda sambamba na ongezeko la madarasa.

Tatizo ni kwamba anasahau kwamba suala la elimu ni mtambuka, kwa maana kwamba kuongezeka kwa ubora wa elimu kunategemea mambo mengine mengi kama vifaa vya kufundishia, vitabu, walimu bora, usafiri, mitalaa sahihi, miundombinu (mabweni, maabara, madarasa) na huduma za maji, afya, nishati, chakula na kadhalika.

Pamoja na kuwapo umuhimu wa kupanua elimu ya msingi kuwa kidato cha nne, tunadhani pia wakati umefika wa kubadilisha mitalaa ili ijikite katika kutoa elimu ya kujitegemea.

Mkazo uwekwe katika elimu ya ufundi, kwa maana ya kuhakikisha angalao kila wilaya inakuwa na chuo kimoja cha kutoa elimu stadi mfano wa VETA. Vinginevyo, majeshi tunayozalisha kila mwaka kutoka shule za msingi yatasababisha  maafa na tutabaki kulia na kusaga meno.

Thursday, September 12, 2013

WFP SASA KUWAWEZESHA WANAFUNZI KUPATA CHAKULA CHA MCHANA.
















Mpango wa Chakula Duniani (WFP), umejitoa katika ufadhili wa uji wa lishe kwenye shule za msingi 1,167 zilizopo Mikoa ya Dodoma, Shinyanga, Singida, Simiyu, Manyara na Arusha.

Akizungumza katika mahojiano mjini Dodoma, Mkuu wa Ofisi ya WFP Mkoa wa Dodoma, Nima Sitta alisema utaratibu huo umeachwa kwa wazazi.

Alisema WFP hivi sasa imejikita katika kuwawezesha watoto waliopo katika shule hizo kupata chakula cha mchana.

Tangu mwaka 2001 WFP imekuwa ikifadhili utoaji ujilishe na chakula cha mchana kwa wanafunzi wa shule hizo ili kupunguza idadi ya watoto wanaoacha shule na kuongeza ufaulu.

“Juzi nilitembelea baadhi ya shule Singida kuangalia jinsi wazazi walivyoweza kuanza kuchangia chakula kwa watoto wao, nikakuta wamefanya vizuri. Kuna shule wazazi wamechangia nafaka za uji hadi Julai mwakani,” alisema.

Hata hivyo, alisema bado Serikali haijaandaa mwongozo wa kuwezesha shule kujitegemea kwa chakula na kwamba mpango mkakati unaotumika ni ule wa WFP.

Katika matembezi ya mshikamano yaliyoandaliwa na WFP kwa ajili ya kuchangia chakula shuleni mwaka juzi, Serikali iliahidi kuanza kutoa chakula shuleni lakini hadi sasa hakuna mwongozo ulioandaliwa.

Monday, September 9, 2013

PICHA ZA MAHAFALI YA SHULE YA SEKONDARI MLONGWEMA ILIYOPO WILAYANI LUSHOTO

















Mwenyekiti Wa Uvccm Mkoa Wa Tanga,Abdi Makange Aliyevaa Kaunda Suti Ya Rangi Ya Bluu Mpauko Katikati Pamoja Akiwasili Eneo La Mahafali Katika Shule Ya Sekondari Mlongwema,Wilayani Lushoto

















Mwenyekiti Wa Uvccm Mkoa Wa Tanga,Abdi Makange Aliyevaa Kaunda Suti Ya Rangi Ya Bluu Mpauko Katikati Pamoja Na Meza Kuu Wakiteta jambo 

















Baadhi ya wanafunzi wahitimu wa shule ya sekondari Mlongwema