Search This Blog
Friday, May 3, 2013
MIMI NA MWANAFUNZI KUPAA NA AZAM UNGA BORA PLUS
Brand Manajer wa kipindi cha Mimi na Mwanafunzi Seleman Kibugo akiashiria ujio wa Azam katika kipindi hicho kinachorushwa kila siku za jumamosi saa tatu asubuhi kupitia Radio Mwambao fm Tanga
NECTA YAAGIZWA KUWEKA VIWANGO ILI MATOKEO YA KIDATO CHA NNE 2012 YALINGANE NA JUHUDI ZAO
Serikali imechukua
uamuzi mgumu na kuamua kuwafariji wanafunzi waliofeli mitihani ya kuhitimu
kidato cha nne mwaka 2012 baada ya kufuta matokeo hayo na kuamua yaandaliwe
upya kwa kutumia utaratibu uliotumika mwaka 2011.
Uamuzi huo wa Serikali
umetokana na matokeo mabaya ya mitihani huo yaliyosababisha zaidi ya asilimia
60 ya wanafunzi kupata sifuri.Kutokana na matokeo hayo, Serikali iliunda Tume
inayoongozwa na Profesa Sifuni Mchome kuchunguza matokeo hayo ili kupata
ufumbuzi wa kudumu.Muda mfupi baada ya tamko la Serikali, baadhi ya wadau wa
elimu wameeleza kufurahishwa na uamuzi huo, huku Chama cha Walimu Tanzania (CWT)
kikiikosoa hatua hiyo, kuwa imekiuka sheria na kupora madaraka ya Baraza la
Mitihani Tanzania (Necta).
Akitoa kauli ya
Serikali bungeni kuhusu taarifa ya awali ya Tume ya Taifa ya Kuchunguza Matokeo
ya Mtihani wa Taifa Kidato cha nne mwaka 2012 jana, Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Waziri Mkuu (Uratibu na Bunge), William Lukuvi alisema wameagiza Necta kuweka
viwango ili matokeo ya wanafunzi yalingane na juhudi zao.
“Standardization
ifanyike ili matokeo ya wanafunzi yalingane na juhudi wazizoziweka katika
kusoma kwa mazingira, hali halisi ya Tanzania na uamuzi wa taifa kuongeza idadi
ya shule na wanafunzi wakati uwekezaji katika ubora unaendelea,” alisema
Lukuvi.
Lukuvi alisema Necta
imeelekezwa kuwa licha ya sheria ya kuanzishwa kwake kuruhusu kufanya
marekebisho ya mchakato wa mtihani, marekebisho yoyote ya kubadilisha utaratibu
wa kupanga viwango vya ufaulu na madaraja ya mitihani yanatakiwa yahusishe
wadau wote wanaohusika na mitalaa, ufundishaji na mtihani.“Wakati Tume
inaendelea kukamilisha kazi yake, uamuzi wa Necta kutumia taratibu mpya wa
kupanga viwango vya ufaulu na madaraja ya matokeo ya mitihani uliotumika 2012
usitishwe,” alisema Lukuvi na kuongeza
“Badala
yake Necta itumie utaratibu uliotumika mwaka 2011 kwa kidato cha nne na sita
kwa mitihani yote, ikiwamo utaratibu wa Standardization na kutoa matokeo mapya
kwa kuzingatia maelekezo haya.”Pia, Serikalli imeagiza mchakato wa tuzo wa
taifa (National Qualifications
Framework)
na Mfumo wa Kutahiniwa/ kuthamini maendeleo ya mwanafunzi masomo yake (National
Assessment Framework) ukamilishwe haraka iwezekanavyo.Katika mtihani wa mwaka
2012, wanafunzi 367,756 walifanya mtihani huo na waliofaulu ni 126,847.
Waliofaulu kwa kwa madaraja ya kwanza hadi la tatu ni 23,520 sawa na asilimia
6.4 na daraja la nne ni 103,327 sawa na asilimia 28.1, huku 240,909 ambao ni
asilimia 65.5 wakipata daraja sifuri.
Wednesday, May 1, 2013
MKUU WA WILAYA YA MKINGA ASEMA UTOAJI WA CHAKULA MASHULENI UTASAIDIA KUPUNGUZA UTORO NA KUFANYA MAHUDHURIO YA WANAFUNZI KUWA MAZURI
IMEELEZWA kuwa utoaji wa chakula mashuleni utasaidia kupunguza utoro na kufanya mahudhurio ya wanafunzi kuwa mazuri ikiwemo kupanda kiwango cha taaluma kwani watoto watakuwa na nguvu ya kusoma na kuelewa watakachokuwa wakifundishwa.
Rai hiyo ilitolewa na Mkuu wa wilaya ya Mkinga, Mboni Mgaza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya utoaji wa chakula kwa wanafunzi iliyofanyika Duga Maforoni na Maramba ambapo alisema anaamini ulaji wa chakula mashuleni utakuwa endelevu na kuwataka wazazi na viongozi kushirikiana na walimu ili kufanikisha suala hilo.
Mgaza alisema katika kufanikisha zoezi hilo la utoaji wa chakula wazazi na wadau wachangie kwa kiasi ambacho kitakuwa kikihitajika kwa kila mtoto kwani watakapopata chakula mashuleni itasaidia pia kuimarisha afya ya watoto wao.
Aidha Mgaza aliwashauri wazazi wilayani humo kujitahidi kuwapeleka watoto wao shuleni ili kuweza kuepuka gharama ambazo zitaweza kuwakuta baade kwani zitakuwa kubwa kuliko wanavyokuwa wakifiria.
Hata hiyo mkuu huyo wa wilaya alisisitiza suala la uvaaji vya viatu mashuleni ambapo alisema tatizo la watoto kukosa viatu linapaswa kuangaliwa na wazazi kwa kuhakikisha kila mtoto wake anavaa viatu ili kuweza kuwaepusha na magonjwa ambayo huenda wakayakuta wakati wakiwa beya.
Awali akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Afisa Elimu wilayani humo, Juma Mhina alisema wanaamini zoezi la uhamasishaji lishe shuleni kwa kushirikiana na wenyeviti wa vijiji na wazazi litaweza kupata mafanikio makubwa.
Mhina alisema wanaamini mpaka ifikapo mwezi wa saba mwaka huu shule zote zilizopo wilayani humo zitakuwa zinapata chakula cha mchana mashuleni ambapo alisema lengo la kampeni hiyo ni kuwawezasha wanafunzi kusoma kwa bidii na kuweza kuelewa wanachofundishwa.
Subscribe to:
Posts (Atom)